Skip to main content

Wanawake Wapewa Adhabu ya Kuchimba Kaburi na Kijiji





Ni kawaida na ni utamaduni wa sehemu nyingi duniani wanaume kuchimba kaburi na kuwaachia wanawake shughuli nyingine za jikoni wakati wa msiba.

Lakini sivyo ilivyokuwa kwa wanawake wa Mtaa wa Bwihegule wilayani Geita. Wanawake hao wa Kata ya Mtakuja walilazimika kuchimba kaburi, ikiwa ni adhabu iliyotokana na tuhuma kuwa wanahusika na vifo vya ghafla vya wanaume mtaani hapo.

Tukio hilo lililoibua hisia na maoni mchanganyiko kutoka kwa walioshuhudia lilitokea Aprili 24 baada ya mkazi wa mtaa huo, Nkangiko Vigume (57), kufariki dunia ghafla Aprili 23.

Wanaume saba wafariki

Habari kutoka mtaani hapo zinasema amri ya kutaka wanawake kuchimba kaburi na kulala matanga ilitolewa na mtemi, ambaye ni kiongozi wa mila wa jamii ya Wasukuma mtaani hapo, Kahema Nsabilando.

Alitoa amri hiyo baada ya uamuzi kufikiwa kwenye kikao cha dharura kilichojadili matukio ya vifo vya ghafla vya wanaume mtaani hapo.

Wakazi waliitisha kikao hicho kujadili vifo vya ghafla vya wanaume baada ya Vigume kufariki Aprili 23 na kufanya idadi ya waliokufa kufikia saba.

“Hili ni tukio la saba wanaume wanafariki ghafla hapa mtaani kwa kuumwa kichwa. Vikao vya wananzengo vimeshafanyika na kuwaonya akina mama kuacha mambo haya (ya kuhusika na mauaji ya kishirikina ya wanaume), lakini wamerudia tena,” alisema Nsabilando.

“Tumechoshwa na lazima waadhibiwe kwa kuachwa walale matanga na kuchimba kaburi wenyewe kwa mujibu wa mila na desturi.”

Kifo na matukio ya ajabu

Akisimulia yaliyojiri kabla ya kikao kilichotoa uamuzi, Nsabilando alisema baada ya Vigume kufariki dunia, utaratibu wa kuandaa mwili kwa ajili ya mazishi ulifanyika lakini yalitokea matukio aliyodai ni ya ajabu yakiashiria kifo chake hakikuwa cha kawaida.

“Wazee tuliuandaa mwili wa marehemu na kuulaza kitandani mikono ikiwa imenyooshwa, lakini baada ya muda mfupi tuliona mikono imewekwa kifuani,” alidai.

Kiongozi huyo alidai kilichowashtua zaidi hadi kufikia uamuzi wa kutoa adhabu ni mwili huo kukutwa umelala kifudifudi licha ya kuachwa kitandani ukiwa chali.

Kuhusu vifo tata mtani hapo, Mbares Mabula ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maafa, alisema ndani ya miaka miwili kumekuwa na vifo vyenye utata vya wanaume vinavyosadikiwa kusababishwa na wanawake wanaotuhumiwa kutaka kutaka kurithi mali.

Alidai baadhi ya waliokufa na kuzikwa, wanaonekana mitaani katika mazingira yanayotatanisha, hivyo kuibua hofu ya ushirikina.

Licha ya mwandishi wa Mwananchi kuwashuhudia polisi wanne katika eneo la tukio, wawili kati yao wakiwa na silaha, kamanda wa polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema jana kuwa ofisi yake haina taarifa hizo.

Lakini mkuu wa wilaya, Herman Kapufi alisema uchunguzi wa awali umebaini limesababishwa na imani potofu za kimila na kuahidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.

“Hivi ni vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake. Serikali haiwezi kuvivumilia, tutafanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya walioamuru wanawake kuchimba kaburi ili kuvikomesha,” alisema Kapufi.

Kapufi alisema imani za kishirikiana huchochea mauaji ya watu kwa kukatwa kwa mapanga katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Wanawake walonga

Baadhi ya wanawake waliofanya adhabu hiyo hawakukubaliana na uamuzi huo.

“Hatukubaliani na uamuzi, lakini hatuna la kufanya kutokana na mabavu ya wanaume ambao baadhi hutushurutisha kwa fimbo kuchimba kaburi,” alisema Specaoza Salum, mmoja wa wanawake walioshiriki kuchimba kaburi.

Mwanamke mwingine, Kabula Shija alisema pamoja na kulala matanga na kukamilisha uchimbaji kaburi kabla ya saa 7:00 mchana siku hiyo ya Aprili 24, wanaume hao pia waliwaagiza kuhakikisha wanapika na kuwapa chakula kabla ya muda huo.

Mwanamke mwingine, Suzan Mayala alisema adhabu hiyo haikujali hali zao kiafya wala majukumu ya kifamilia na kijamii kwa sababu ilihusisha wanawake wote wakiwemo wenye watoto wachanga.

Familia haikuweza kuzuia

Hata kama isingekubaliana na adhabu hiyo, familia ya wafiwa haikuwa na uwezo wa kuzuia utekelezaji wake.

Thomas Nzobano, kiongozi wa ukoo wa marehemu Vigume, alisema hawakuwa na uwezo wa kuingilia kati uamuzi wa wananzengo kwa sababu kiutaratibu hawaruhusiwi kujihusisha na masuala ya matanga na mazishi.

“Familia tunatakiwa kusubiri uamuzi na kufuata maagizo ya wananzengo kuhusu masuala yote ya mazishi. Hatujihusishi na kuchimba kaburi kwa kuwa hiyo ni kazi ya wanajamii,” alisema Nzobano.

Mwanafamilia mwingine, Ndakirwa Mkangiko ambaye ni mmoja wa watoto 12 wa Vigume, alisema familia imeshtushwa na kifo cha ghafla cha baba yao aliyeugua kichwa kwa muda mfupi.

Hasira zilizidi nguvu uongozi

Mwenyekiti wa Mtaa ya Bwihegule, Andrea Barnaba alisema hamaki na hasira ya wananchi kuhusu matukio ya vifo na madai ya mwili wa marehemu kugeuzwa ulipolazwa, ziliuzidi nguvu uongozi wa Serikali ya eneo hilo na kulazimika kuwaacha wananchi kuendelea na walichoamua.

“Hakuna mtu wala kiongozi yeyote aliyekuwa akisikilizwa na wananchi zaidi ya viongozi wa kimila wakiongozwa na mtemi. Kama viongozi tuliona ni busara kutotumia mabavu ili kuepuka madhara zaidi kutokana na hamaki waliyokuwa nayo wananchi,” alisema Barnaba.

Comments

Popular posts from this blog

Historia ya mkoa wa kigoma

 Mkoa wa Kigoma  uko kati ya mikoa 31 ya Tanzania wenye postikodi namba 47000. Umepakana na Burundi na Mkoa wa Kagera upande wa Kaskazini, mikoa ya Shinyanga na Tabora upande wa mashariki na Mkoa wa Rukwa upande wa kusini. Magharibi umepakana na Ziwa Tanganyika penye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Viwianishi: 4°53′S 29°40′E / 4.883°S 29.667°E Nchi Tanzania Wilaya 8 Mji mkuu Kigoma Serikali - Mkuu wa Mkoa Emmanuel Maganga Eneo - Mkoa 46,066 km² - Bara 37,037 km² - Maji 8,029 km² Idadi ya wakazi (2012) - 2,127,930 Jiografia Mkoa una eneo la km² 45,066 (sawa na 4.8% ya eneo lote la Tanzania) ikiwa km² 8,029 ndizo maji ya ndani (hasa Ziwa Tanganyika) na km² 37,037 ndizo nchi kavu. Takriban robo ya eneo la mkoa wa Kigoma hutumika kwa kilimo na ufugaji, karibu nusu ni misitu. Kwa ujumla eneo la mkoa ni tambarare ya juu inayoanza kwenye mita 800 juu ya UB karibu na Ziwa Tanganyika na kupanda hadi mita 1,750. Mito ya kudumu ndani ya mkoa wa K...

UK yawatahadharisha Watanzania Kuhusu Maandamano Ya Tarehe 26/04/2018

                London, Uingereza. Serikali ya Uingereza imewataka wananchi wake wanaoishi hapa nchini kuchukua tahadhari na maandamano ya kisiasa yanayotarajiwa kufanyika Aprili 26. Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Aprili 24 imesema kwamba kuna raia zaidi ya 75,000 wanaoingia nchini hapa kila mwaka. Hivyo imewatahadharisha kujihusisha na maandamano hayo kwa madai kwamba wanaweza kupata madhara kutoka kwa jeshi la polisi. Katika taarifa hiyo ilitolewa tahadhari kwamba kwa sababu maandamano hayo yalishapigwa marufuku hivyo polisi ni lazima watatumia mabomu ya machozi au silaha za moto. “Hivyo muwe makini sana mnapokuwa kwenye mizunguko yenu muepuke mikusanyiko ya watu au watu wanaoandamana, muda wote muwe mnasikiliza vyombo vya habari, mjue nini kinachoendelea,’’ ilisema taarifa hiyo na kuongeza: “Ikiwa mnahitaji mawasiliano na namba ya dharura ya kupiga haraka ni 112 uliza huduma ya d...

Mbwa Atunukiwa ‘Tuzo ya Polisi ya Heshima’ kwa Kumlinda Mtoto Aliyepotea

Kisa kimoja kimezua hisia huko nchini Australia baada ya mbwa mmoja mzee aitwaje Max kukaa na kumlinda mtoto mdogo ambaye alipotea kutoka nyumbani kwao kwa saa 15.  Inaelezwa kuwa mtoto huyo aliondoka akiwa anacheza tu na kutoweka kwa saa 15 huku akizua taharuki kwa ndugu na watu mbalimbali kumtafuta na baadaye kumpata porini akiwa na mbwa huyo Max.  Kwa saa zote hizo mtoto huyo wa miaka mitatu anayejulikana kwa jina la Aurora alikuwa na mbwa katika vichaka vya eneo la Queensland’s Southern Downs.  Baada ya kumpata mtoto polisi waliokuwa kwenye msako na ndugu, walimpa mbwa huyo heshima ya kuwa ”mbwa wa polisi wa heshima’ kwa kumlinda mtoto huyo.