Mkoa wa Kigoma uko kati ya mikoa 31 ya Tanzania wenye postikodi namba 47000. Umepakana na Burundi na Mkoa wa Kagera upande wa Kaskazini, mikoa ya Shinyanga na Tabora upande wa mashariki na Mkoa wa Rukwa upande wa kusini.
Magharibi umepakana na Ziwa Tanganyika penye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Viwianishi: 4°53′S 29°40′E / 4.883°S 29.667°E
Nchi
Tanzania
Wilaya
8
Mji mkuu
Kigoma
Serikali
- Mkuu wa Mkoa
Emmanuel Maganga
Eneo - Mkoa 46,066 km² - Bara 37,037 km² - Maji 8,029 km² Idadi ya wakazi (2012) - 2,127,930
Jiografia
Mkoa una eneo la km² 45,066 (sawa na 4.8% ya eneo lote la Tanzania) ikiwa km² 8,029 ndizo maji ya ndani (hasa Ziwa Tanganyika) na km² 37,037 ndizo nchi kavu.
Takriban robo ya eneo la mkoa wa Kigoma hutumika kwa kilimo na ufugaji, karibu nusu ni misitu.
Kwa ujumla eneo la mkoa ni tambarare ya juu inayoanza kwenye mita 800 juu ya UB karibu na Ziwa Tanganyika na kupanda hadi mita 1,750. Mito ya kudumu ndani ya mkoa wa Kigoma ni Malagarasi, Luiche, Ruchugi na Rugufu.
Hifadhi za wanyama na za kihistoria Kuna maeneo mawili yenye sokwe: ndipo Hifadhi ya Taifa ya Gombe (alikofanya utafiti wake mwanabiolojia Jane Goddall) na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale.
Utawala
Kuna wilaya nane ambazo ni (idadi ya wakazi katika mabano): Kigoma Mjini (144,852), Kigoma Vijijini (490,816), Kibondo (414,764), Kasulu (628,677), Uvinza (383,640), Buhigwe (254,342) na Kakonko (167,555) . Jumla ya wakazi ni 2.127.930 (sensa ya mwaka 2012).
Makao makuu ya mkoa ni Kigoma mjini. Mji wa Ujiji ulioko karibu na Kigoma mjini ndio mji wa kale zaidi katika Tanzania ya Magharibi penye makumbusho ya David Livingstone.
Wakazi
Kabila kubwa ni Waha, likifuatwa na Wabembe Watongwe na Wamanyema. Kuna pia Wanyamwezi, Wasukuma, Wafipa na watu wenye asili ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Idadi au msongamano wa watu katika maeneo ya mkoa huu imetegemea sana shughuli zinazofanyika kama vile kilimo na uvuvi pamoja na kupatikana kwa nzi aina ya ndorobo: penye ndorobo wengi huwa na watu wachache.
Uchumi na mawasiliano
Mkoa wa Kigoma bado hauna maendeleo yanayolingana na mazingira yake. Hali ya barabara na mawasiliano mengine ni mbaya. Umbali hadi Dar es Salaam ni km 1316, hadi Mwanza 830, hadi Arusha 1204. Lakini hakuna barabara ya lami hata barabara za kokoto ni sehemu ndogo tu.
Usafiri muhimu ni reli kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kupitia Tabora na Dodoma.
Isipokuwa reli hii imeshazeeka kutokana na kujengwa zamani za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Treni (gari moshi) zake huchelewachelewa kwa kuchukua muda mrefu.
Wakati wa mvua inatokea ya kwamba mawasiliano yanavurugika. Uwanja wa ndege wa Kigoma inashughulika ndege ndogo aina ya Fokker.
Takribani 85% ya wakazi wote hutegema kilimo, walio wengi kilimo cha kujitegemea tu, tena cha jembe la mkono.
Kuongezeka kwa wakimbizi kutoka nchi jirani na kukua kwa makambi kulikuwa tatizo kubwa.
Majimbo ya bunge
Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo: Buyungu : mbunge ni Bilago Samson (Chadema) Kasulu Mjini : mbunge ni Daniel Nsanzugwako (CCM) Kasulu Vijijini : mbunge ni Augustine (CCM) Kigoma Kaskazini : mbunge ni Peter Serukamba (CCM) Kigoma Kusini/Uvinza : mbunge ni Hasna Mwilima (CCM) Kigoma Mjini : mbunge ni Zitto Z. Kabwe (ACT-Wazalendo) Manyovu : mbunge ni Albert Ntabaliba (CCM) Muhambwe : mbunge ni Atashasta Justus Nditiye (CCM) .
Comments
Post a Comment