Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ipo kwenye majadiliano ya kuhamisha kituo cha Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), kilichopo Jangwani na kukipeleka kwenye kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani Ubungo (UBT).
Hatua hiyo inatokana na eneo hilo la Jangwani kukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara hali inayosababisha kuharibika kwa magari hayo.
Akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha madiwani jana, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, alisema uamuzi huo umefikiwa ili kunusuru magari hayo yasiendelee kuharibika.
Alisema Menejimenti ya Kampuni ya UDART na viongozi wa jiji wapo kwenye majadiliano kuhusu suala hilo ili waweze kufikia mwafaka.
“Kwa sasa tupo kwenye majadiliano kwa ajili ya kuhamisha kituo cha mabasi yaendayo kasi(UDART) cha Jangwani tuweze kukipeleka Ubungo kwa sababu eneo la Jangwani limekuwa likikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara mvua inaponyesha,”alisema Mwita.
Alisema suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na Halmashauri ya Jiji hilo ipo kwenye mchakato wa kupanua Mto Msimbazi uweze kuwa na nafasi kubwa ya kusafirisha maji hadi baharini.
Meya alisema jambo hilo linaweza kupunguza mafuriko katika eneo la Jangwani na maeneo karibu na mto huo.
Alisema fedha za upanuzi huo zimekwisha kutolewa, kilichobaki ni utekelezaji wa mradi kuanzia daraja la Salendar hadi Pugu.
“Awamu ya kwanza ya mradi itaanzia Salendar hadi Kigogo, jambo ambalo linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo la mafuriko kwa wakazi wa Jangwani na maeneo jirani ya mto Msimbazi,” alisema.
Vilevile, Meya Mwita alisema Serikali Kuu imetoa shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa çha mabasi yaendayo mikoani, kitakachojengwa Mbezi Mwisho.
Alisema licha ya kutolewa kiasi hicho cha fedha, jiji limetoa shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi ambao maeneo yao yatachukuliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
“Tunatarajia kupata ekari 24 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha Mbezi Mwisho, ujenzi ambao utaanza wakati wowote kuanzia sasa. Mkakati uliopo ni kuwalipa fidia wananchi wa eneo lile tuweze kuendeleza mradi,” alisema.
Alisema mradi huo utachukua miaka miwili kukamilika na ndani yake kutakua na maduka na nyumba za kulala wageni, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kuongeza mapato.
Alisema mwaka huu katika makusanyo yake ya kila mwaka, halmashauri imeingiza shilingi bilioni 22 ambazo zitatumika kwa mambo mbalimbali yakiwamo uendelezaji wa miradi.
Chanzo: Swahili Times
========
Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam ipo kwenye majadiliano ya kuhamisha kituo cha mabasi yaendayo haraka (UDART), kilichopo Jangwani na kupeleka kwenye kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo UBT, kutokana na eneo hilo la Jangwani kujaa maji kila mara wakati mvua zinaponyesha.
Comments
Post a Comment