Klabu ya soka ya Azam FC imetua mkoani Morogoro kwaajili ya kuweka kambi kuelekea mchezo wake dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa kesho huku pia klabu za SImba na Yanga zikiwa zimeweka kambi mkoani humo.
Azam FC imeondoka jijini Dar es salaam ikiwa tayari imeshafanya maandalizi yote ya mchezo huo na kitakachofanyika katika kambi ya muda mfupi Morogoro ni mazoezi mepesi tu kabla ya mechi.
Jumanne hii Azam FC ilicheza mchezo wa kirafiki na Kombaini ya Jeshi na kushinda mabao 2-0 yaliyofungwa na mshambuliaji Shaaban Idd na winga Enock Atta. Mchezo huo ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya kesho.
Timu hizo zilipokutana kwenye raundi ya kwanza zilitoka sare ya bao 1-1, Azam FC ikitangulia kufunga kupitia kwa winga Enock Atta kabla ya Kelvin Sabato kusawazisha dakika za mwisho kwa mpira wa moja kwa moja wa adhabu ndogo.
Hadi sasa kwenye msimamo wa ligi, Azam FC inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46 huku wapinzani wao Mtibwa Sugar ikiwa nafasi ya sita kwa pointi 33. Simba na Yanga nazo zipo Morogoro kumalizia maandalizi ya mchezo wao wa Jumapili.
Comments
Post a Comment