Skip to main content

Lowasa asema hatapoteza muda kupima DNA

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema hamtambui mwanamke aliyejitambulisha juzi kama binti yake aliyetelekezwa na kwamba hatapoteza muda kwenda kupimwa vinasaba (DNA), kama msichana huyo alivyotaka.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam kwa njia ya simu, Lowassa ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kuwa kinachofanyika kwenye zoezi hilo ni siasa.

Msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma alijitokeza hadharani juzi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kudai kutelekezwa na Lowassa ambaye alisema ni baba yake, kwa kuambiwa na mama yake mzazi.
"Wewe unamwamini kweli huyo msichana? Angekuwa mwanangu kweli ningeshamchukua muda mrefu, kwanza wala simjui naona siasa zinaingizwa hapo," alisema.

Alipoulizwa kama yuko tayari kupimwa DNA ili ukweli ujulikane, Lowassa alijibu "Kupima DNA huo ni upuuzi. Yaani nipoteze muda wangu kwenda kufanya upuuzi huo? Siko tayari."

Msichana huyo ni miongoni mwa mamia ya wanawake waliojitokeza kuanzia Jumatatu kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda.

Makonda alitaka wanawake waliotelekezewa watoto na waume zao wafike ofisini kwake kwa siku tatu kuanzia Jumatatu, kwa ajili ya kuzungumza na wanasheria, maofisa wa ustawi wa jamii na askari polisi wa Dawati la Jinsia. Siku hizo zitaisha kesho baada ya kuongezwa.

Akizungumza na vyombo vya habari juzi, Fatuma alisema yuko tayari kupima vinasaba na Lowassa ili kuthibitisha kama kweli ni baba yake na kwamba alimtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio. "Nilipeleka barua Ikulu kuomba kuonana na baba (Lowassa) kipindi akiwa Waziri Mkuu (2006-2008) lakini niliitwa mimi na mama katika klabu ya Mamba iliyopo Kinondoni," alisema Fatuma.

"(Hapo) alikuja mwanaume akiwa kwenye gari lenye vioo vyeusi akatuhoji mimi na mama, akaondoka hakutupa majibu yoyote hadi leo.

" Kuhusu madai hayo, Lowassa alisisitiza kuwa kama kweli angekuwa mtoto wake asingesita kumchukua.

"Wala simjui, anasema ameshindwa kuniona wakati ana miaka 31, wewe unaamini kweli ameshindwa kuniona? Mbona wewe umenitafuta na umenipata na unaongea na mimi kwenye simu," alisema Lowassa.

"Hizo ni siasa zinazolenga kuchafuana."

Pia katika maelezo yake, Fatuma alidai kuwa aliwahi kukutana na mtoto wa Lowassa aitwaye Fred na alimwahidi kumsaidia lakini hadi sasa amekuwa kimya.

FURIKA VIWANJANI
Katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, mamia ya wanawake walifurika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuanzia saa 11 alfajiri ili kupata namba.

Kutokana na mwitikio kuwa mkubwa, wanawake waliofika kuanzia saa 1:00 asubuhi walikuwa hawajapata namba hadi saa 8:00 mchana, huku waliojiandikisha wakiwa zaidi ya 500.

Hata mvua iliyoanza kunyesha majira ya saa 6:00 mchana ikiambatana na radi haikuwazuia wanawake wakiwa na watoto wao wadogo wa chini ya miaka mitatu kuendelea kupanga foleni kusubiri huduma.

Baadhi ya wanawake hao walilazimika kuingia gharama za kununua miavuli ili kujisitiri na mvua hiyo ili kutimiza kusudi lillilowapeleka eneo hilo.

Kutokana na mwitikio mkubwa wa wanawake hao, Makonda alilazimika kuongeza siku za kuwahudumia kutoka tatu zilizokuwa zimepangwa hadi kufikia tano.

Makonda alisema wanawake hao watapatiwa msaada wa kisheria kila mmoja ndani ya siku hizo tano na kwamba wanaume watakaotajwa kuhusika kuwatelekeza wataitwa kuhojiwa. Walishaanza kuitwa.

Alisema wanaume watakaotajwa watatakiwa kufika katika ofisi hizo kueleza sababu za kutelekeza watoto na endapo kutakuwepo na utata kuhusu uhalali wa mtoto vipimo vya Vinasaba vya Binadamu (DNA) vitatumika.

Kadhalika, aliahidi kuwatangaza wanaume watakaokaidi kuwatunza watoto wao ili jamii iwatambue.

"Tutangaza majina ya wanawaume wote wataotajwa kuhusika na hawa watoto ili jamii iwatambue," alisema Pia aliwatia moyo wanawake hao kwa kusema tendo la kuzaa si tendo la laana bali ni tendo la baraka na kila mmoja anatakiwa kuliheshimu.

Comments

Popular posts from this blog

Historia ya mkoa wa kigoma

 Mkoa wa Kigoma  uko kati ya mikoa 31 ya Tanzania wenye postikodi namba 47000. Umepakana na Burundi na Mkoa wa Kagera upande wa Kaskazini, mikoa ya Shinyanga na Tabora upande wa mashariki na Mkoa wa Rukwa upande wa kusini. Magharibi umepakana na Ziwa Tanganyika penye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Viwianishi: 4°53′S 29°40′E / 4.883°S 29.667°E Nchi Tanzania Wilaya 8 Mji mkuu Kigoma Serikali - Mkuu wa Mkoa Emmanuel Maganga Eneo - Mkoa 46,066 km² - Bara 37,037 km² - Maji 8,029 km² Idadi ya wakazi (2012) - 2,127,930 Jiografia Mkoa una eneo la km² 45,066 (sawa na 4.8% ya eneo lote la Tanzania) ikiwa km² 8,029 ndizo maji ya ndani (hasa Ziwa Tanganyika) na km² 37,037 ndizo nchi kavu. Takriban robo ya eneo la mkoa wa Kigoma hutumika kwa kilimo na ufugaji, karibu nusu ni misitu. Kwa ujumla eneo la mkoa ni tambarare ya juu inayoanza kwenye mita 800 juu ya UB karibu na Ziwa Tanganyika na kupanda hadi mita 1,750. Mito ya kudumu ndani ya mkoa wa K...

Stendi ya mabasi ya mikoani Ubungo kuhamishwa kupisha kituo cha mabasi ya Mwendo Kasi

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ipo kwenye majadiliano ya kuhamisha kituo cha Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), kilichopo Jangwani na kukipeleka kwenye kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani Ubungo (UBT). Hatua hiyo inatokana na eneo hilo la Jangwani kukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara hali inayosababisha kuharibika kwa magari hayo. Akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha madiwani jana, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, alisema uamuzi huo umefikiwa ili kunusuru magari hayo yasiendelee kuharibika. Alisema Menejimenti ya Kampuni ya UDART na viongozi wa jiji wapo kwenye majadiliano kuhusu suala hilo ili waweze kufikia mwafaka. “Kwa sasa tupo kwenye majadiliano kwa ajili ya kuhamisha kituo cha mabasi yaendayo kasi(UDART) cha Jangwani tuweze kukipeleka Ubungo kwa sababu eneo la Jangwani limekuwa likikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara mvua inaponyesha,” alisema Mwita. Alisema suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na Halmashauri ya Jiji hilo ipo kwenye mchakato wa kupanua Mt...

Mabasi ya Mwendokasi yasitisha huduma zake kwa muda

Kampuni inayotoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (UDART) imeamua kusitisha usafirishaji wa abiria kwa baadhi ya njia kuanzia saa 6:00 mchana kutokana na kufungwa kwa barabara ya Morogoro eneo la Jangwani kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.  Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano UDART, Deus Bugaywa na kusema wamechukua maamuzi hayo kutokana na maji mengi ya mvua kupita juu ya daraja la Mto Msimbazi Jijini Dar es Salaam hali ambayo inahatarisha usalama wa abiria pamoja na vyombo vya usafirishaji.  "Kwa sasa huduma zinatolewa kwa njia za Mbezi - Kimara, Kimara - Morroco, Kimara - Magomeni Mapipa, Kivukoni - Muhimbili, Gerezani - Kvukoni, na Gerezani - Muhimbili. Huduma kamili zitarejea mara baada ya barabara kufunguliwa", amesema Bugaywa. Kwa upande mwingine, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano UDART, Deus Bugaywa amewaomba radhi wananchi wanaotumia usafiri huo kwa usumbufu ambao utajitokeza kwa namna moja ama ny...