Haruna Niyonzima KIUNGO wa Simba, Haruna Niyonzima amenusurika katika ajali aliyoipata eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.
Niyonzima amepata ajali hiyo juzi baada ya gari lake kupiga bonde na kupoteza mwelekeo wakati akirejea nyumbani kwake. Taarifa zinaeleza Niyonzima raia wa Rwanda alikuwa mwenyewe kwenye gari na akiwa njiani wakati anarejea nyumbani, akakutana na majanga hayo.
Jana Championi juhudi za kumpata Niyonzima aliyetua nchini kuichezea Yanga akitokea APR ya Rwanda na baada ya kumpata alithibitisha kupata ajali na kusema anamshukuru Mungu kwa kuwa haikuwa ajali kubwa.
“Gari lilipoteza mwelekeo wakati nikiwa njiani narejea nyumbani na kuingia kwenye msingi.
Bahati nzuri sikuwa katika mwendo mkubwa na kuna mtu alikatiza ghafla, nilipojaribu kumkwepa nikapoteza mwelekeo wakati najitahidi kurudi barabarani, nikapiga bonde gari likanishinda nikaingia msingini. “Haukuwa msingi mrefu, baadaye walikuja watu tukalitoa nikaondoka.
Nashukuru sikuumia wala yule mtu sikumgonga hivyo hakuna aliyeumia, Gari ilipata mikwaruzo,” alisema.
Taarifa za Niyonzima kupata ajali zilisambaa jana mchana na kila mmoja alikuwa akieleza tofauti zikiwemo taarifa za kwamba aliumia na wengine wakisema alikuwa na rafiki zake.
Lakini Niyonzima alisisitiza alikuwa mwenyewe kwenye gari na taarifa hizo ziliifikia familia yake yeye akiwa nyumbani na baadhi ya watu walisema wamesikia ameumia sana, jambo ambalo halikuwa sahihi.
Niyonzima amejiunga na Simba akitokea Yanga lakini hakuwa na msimu mzuri baada ya kuumia na kulazimika kwenda kutibiwa India.
Hivi karibuni ameanza kurejea taratibu akicheza mechi kwa dakika kadhaa, jambo ambalo limeamsha matumaini upya kwake.
Comments
Post a Comment