Kiwanda cha SIDO mkoani Kigoma kinachojihusisha na uchakataji wa mazao yatokanayo na Mchikichi kipo hatarini kupunguza uzalishaji kutokana na kutokuwa na miundombinu bora.
Meneja wa SIDO mkoani Kigoma Gelevas Mtahaba alielezea alikiri kuwepo kwa changamoto hizo zinazoikabili kiwanda hicho ambacho hutumiwa na wajasiliamali wengi.
“SIDO inategemewa mkoani hapa na wajasiliamali wa zao hili la mchikichi ndio kitega uchumi lakini bado zao hilo halina ubora kuweza kuzalisha mafuta mengi kutokana na wakulima wa zao hili kutokua na elimu juu ya zao hili,” alisema Mtahaba.
Mtahaba alisema ikiwa Sera ya Awamu ya Tano ni Tanzania ya Viwanda mkoa huu uko nyuma katika viwanda japokua wanategemea zao la mchikichi toka enzi za wakoloni, ni vyema wananchi wakaanzisha vikundi vidogovidogo ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu kwa lengo la kuanzisha viwanda vidogo.
Alisema kiwanda hicho cha SIDO ina jumla ya wajasiliamali 300 kutoka kigoma na maeneo ya jirani ambapo hulipa ushuru na kuingiza kipato katika serikali.
Naye moja kati ya wajasiliamali Hamisi Mengi, alisema wanakabilia wa changamoto ya maji machafu yanayotuama katika kiwanda hicho kusababisha harufu mbaya na kuwa kero kwa wajasiliamali katika eneo hilo.
Mengi, alisema usafiri pia ni changamoto inayo wakabili kutoka shambani hadi kiwandani hapo, jambo ambalo linawakatisha tamaa wajasiliamali wengi na wengine kuachana na biashara hiyo.
Alisema ni vyema Serikali ikawekeza katika zao hilo kwani ni zao ambalo huzalisha mafuta ya mawese na sabuni ambazo hutegemewa na ndani ya nchi na kupanua soko katika zao hilo kuliko kuagiza bidhaa nyingine kutoka nchi za nje.
Comments
Post a Comment