Mbunge wa Ukonga (CHADEMA) Mh. Mwita Waitara amehoji uamuzi wa serikali kutangaza kutoa elimu bure licha ya changamoto ambazo bado zinaikumba sekta hiyo nchini na kutaka wananchi waingie gharama za kuchangia elimu isipokua kwa familia maskini.
Waitara amesema hayo jana bungeni Mei 02, 2018 wakati wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuongeza kwamba Tanzania hakuna elimu ya bure bali serikali imepunguza gharama kwa kufuta ada tu.
“Na mimi nimekua nikipinga mara zote Tanzania hakuna elimu ya bure, kuna elimu iliyopunguzwa gharama zake, serikali ilichofanya imeondoa ada lakini mambo mengine yatabaki, natukubaliane mheshimiwa Mwenyekiti haiwezekani taifa hili kila kitu kikatolewa bure watoto watakua wazembe na walemavu” alisema Waitara
Waitara ameongeza kuwa kitendo cha serikali kutangaza elimu bure kinadumaza wananchi na kushindwa kutimiza majukumu yao kama wazazi katika jukumu la kusimamia watoto kielimu na itapelekea Tanzania kuwa ni taifa la watu wavivu.
Serikali ya awamu ya tano ilianza kutoa elimu ya bure katika ngazi ya awali, msingi na sekondari kuanzia mwaka 2016 ikiwa ni utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya 2014 na ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015.
Comments
Post a Comment